Thursday, February 3, 2011

Gavana Ndulu azungumzia noti mpya.




Imeelezwa kuwa hali ya kuacha rangi pindi noti mpya zinaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe ni kwa ajili ya kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa noti kuchanika na kuchakaa haraka.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa BENO NDULU amesema noti inaposuguliwa kwa nguvu kwenye karatasi nyeupe na kuacha rangi ni uthibitisho kuwa noti hiyo ni halali.
Profesa NDULU amesema hali hiyo ni moja ya usalama inayothibitisha kuwa noti hizo ni halali.

Amesema kuwa noti halali zikilowekwa kwenye maji hazichuji kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi kwa kuwa wino uliotumika hauyeyuki katika maji.
Ameongeza kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ya kuwekewa kinga dhidi ya uchafu ili kupunguza uwezekano wa kunasa uchafu inapokuwa katika mzunguko.
Gavana NDULU amewashauri wananchi kuzichunguza kwa makini noti mpya kwa kutumia alama ya usalama ya Mwalimu NYERERE inayoonekana noti inapomulikwa kwenye mwanga ikiwa ni pamoja na kuipapasa ili kuhisi mparuzo kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalum.






Hivi karibuni baadhi ya wananchi wamekuwa na hofu juu ya noti mpya kwa madai kuwa zinachuja rangi hali ambayo imezua utata kwa wananchi wengi.

No comments: