Monday, June 27, 2011

PINDA AWAPASHA WAKUU WA MIKOA, WILAYA NA MA DED

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya wana wajibu wa kuzisimamia Halmshauri zote nchini kuhakikisha kazi ya kuleta maendeleo na kuondoa umasikini inatekelezwa vizuri na Halmashauri zinazingatia thamani ya fedha (Value for Money) katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Mhe. Pinda alikuwa akizungumza katika Semina Elekezi kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwenye Kituo cha Mikutano cha St. Gaspar mjini Dodoma leo (Jumapili Juni 26, 2011) mchana.

Alisema kuwa katika ziara zake za mikoani, amebaini kuwa baadhi ya Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri hawajui wajibu wao na hivyo hoja kwamba Ofisi za Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya zisiwepo haina maana.

“Ukimuondoa RC (Mkuu wa Mkoa), ukimuondoa DC (Mkuu wa Wilaya), basi hakutakuwa na lolote la maana litakalofanyika katika kusimamia maendeleo ya wananchi…Baadhi ya Wakurugenzi hawajui wako hapo walipo kwa ajili gani na wanashindwa kujitambulisha na matatizo ya wananchi ya kuondoa umasikini,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanaweza wakaanzia usimamizi wao kwenye Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuzihoji Halmashauri zimetatua vipi mapungufu yaliyojitokeza na zimetekeleza vipi ushauri wa CAG.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu pia aliwataka Wakuu wa Mikoa kuwa na mfumo wa kutoa habari mara kwa mara kwa Vyombo vya Habari ili umma ufahamishwe shughuli mbalimbali za Serikali na mafaniko yanayopatikana katika utekelezaji wake.

No comments: