Thursday, June 30, 2011

SEHEMU YA TARIFA YA HABARI YA UPENDO FM RADIO LEO

JUNI 30, 2011 PONGEZI 7PM.
DAR ES SALAAM:

Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Bwana, REGINALD MENGI amempongeza Mwenyekiti wa mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote Mama ANNA MKAPA kwa jitihada zake anazofanya kusaidia akinamama wajasiriamali nchini kupitia mfuko huo.

Bwana MENGI ameyasema hayo alipotembelea Banda la Mfuko huo katika maonesho ya 35 ya Biashara ya Kimataifa kwenye Viwanja vya Mwalimu J.K NYERERE Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

MENGI amesema kupitia miradi ya mfuko huo wa fursa sawa kwa wote, Mama MKAPA ameonesha kwa vitendo kuwa kiongozi shupavu aliyetoa muongozo wa kusaidia akinamama wengi kufungua biashara mbalimbali za kujiongezea kipato.

Kuhusu maonyesho hayo, Bwana MENGI amesema tofauti kati ya maonesho ya mwaka huu na miaka iliyopita inaonekana katika ubora wa bidhaa.
Ameeleza kuwa katika maonesho ya mwaka huu wajasiriamali wamejitahidi kuonesha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu hususan kwa wajasiriamali wa Tanzania.

/IS REPORTING 14



JUNI 30, 2011 MAZINGIRA 7PM.
DAR ES SALAAM:

Wadau wa mazingira nchini wametakiwa kutumia taaluma na uzoefu wao kuainisha maeneo ya vipaumbele vya kitaifa kwa ajili ya ufadhili wa mfuko wa mazingira wa dunia.

Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana TUTUBI MANGAZENI amesema hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kuainisha maeneo ya vipaumbele vya kitaifa.

Amehimiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa uwazi na uwajibikaji katika kuainisha maeneo yanayohitaji fedha za utekelezaji kwa kuzingatia vigezo vya dunia na vipaumbele vya kitaifa.
Amesema nia ya mfumo huo ni kuimarisha uwezo wa kila nchi kuainisha vipaumbele vyake ili fedha itakapotolewa iweze kuelekezwa maeneo ambayo ni vipaumbele halisi vya nchi husika.
Maeneo matatu makuu ambayo fedha za mfuko wa mazingira wa dunia utaelekeza ufadhili wake ni katika masuala ya Bionuai, mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa ardhi.

Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira katika ofisi ya Makamu wa Rais Dakta, JULIUS NINGU amehimiza washiriki kuainisha vipaumbele vya taifa kutokana na mahitaji, miongozo na mfumo uliopo na sio kwa matakwa yao.

/SBS REPORTING 15



JUNI 30, 2011 KUUNGANA 7PM.
MORONI.

Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) mama SALMA KIKWETE amewataka Wanawake nchini Comoro kuungana na kutumia fursa za jumuiya mbalimbali walizonazo kujiletea maendeleo.

Amesema maendeleo ya wanawake duniani yanatokana na juhudi zao wenyewe na kusisitiza kuwa umoja na upendo miongoni mwao na kufanya kazi kwa bidii ndiyo msingi ya kujiletea maendeleo.

Akizungumza na wanachama wa Mtandao wa Wanawake na Maendeleo mjini Moroni nchini Comoro Mama KIKWETE amewapongeza wanachama wa mtandao huo kwa malengo mazuri waliyojiwekea ili kuwakomboa wanawake licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi na kuwataka kupanua huduma na mafunzo katika maeneo mengi nchini humo.

Amewakaribisha viongozi wa mtandao huo nchini Tanzania kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuona mafanikio yaliyofikiwa katika Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).

Mke wa Rais wa Comoro Bibi, IKILILOU HADIDJA ABOUBACAR amesema mtandao huo unaolenga zaidi kumkomboa mwanamke na kuimarisha mshikamano wa wanawake katika kutatua matatizo yao ulianzishwa mwaka 1993 na unashirikisha jumuiya takribani 100.


/SBS/AR REPORTING 16


JUNI 30, 2011 POLISI 7PM
DAR ES SALAAM:
Watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti ya ajali yaliyotokea jijiji Dar es Saalam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Saalam SULEIMAN KOVA amewataja watu waliofariki dunia kwenye matukio hayo kuwa ni Bwana YUSUPH MOHAMED mkazi wa Gongo la Mboto na mwingine ambaye bado hajatambuliwa.

Ameeleza kuwa katika tukio la kwanza ambalo limetokea eneo la Ukonga Mombasa, gari aina ya DCM ikitokea Ukonga Mombasa kuelekea Gongo la Mboto limemgonga YUSUPH MOHAMED ambaye ni mfanyabiashara wa Gongo la Mboto, na kufariki dunia wakati akikimbizwa hospitalini.

Katika tukio jingine, gari aina ya Toyota Hilux yenye namba za usajili T 292 ACF ikiendeshwa na dereva JOYCE RWEMBANGIRA kutokea Ubungo Shekilango kuelekea Mabibo imemgonga dereva wa pikipiki yenye namba za usajili T 957 BKM na kufariki papo hapo ambapo mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala.



/CM REPORTING 16




JUNI 30, 2011 BUNGE 7PM
DODOMA:

Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania leo limeendelea na maswali na majibu ikiwa ni mabadiliko yaliyofanywa na Bunge baada ya kuondoa kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa papo yanayopaswa kujibiwa na Waziri Mkuu kila siku ya Alhamisi.

Kutokana na kuahirishwa kwa kipindi hicho cha maswali kwa Waziri Mkuu, mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha, Mbunge wa jimbo la Ubungo Mheshimiwa JOHN MNYIKA aliomba mwongozo wa kutokuwepo kwa kipindi hicho kutoka kwa Mwenyekiti wa Bunge.
Mheshimiwa MNYIKA ameeleza kuwa katika siku za karibuni kumekuwepo na mambo ambayo yanahitaji majibu kutoka serikali hali ambayo itakuwa tofauti iwapo kipindi hicho hakitakuwepo.

Akitoa mwongozo huo baada ya maelezo ya MNYIKA, Mwenyekiti wa Bunge GEORGE SIMBACHAWENE ambaye alikuwa kiongozi wa Bunge katika kikao hicho, ameeleza kwamba kanuni ilitenguliwa ili kumpa fursa Waziri Mkuu kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika masuala ya bajeti ya ofisi yake ya mwaka wa fedha 2011/2012.

/IS REPORTING 18


JUNI 30, 2011 BUNGE 7PM
DODOMA:

Naibu Waziri wa Afya na Ustai wa Jamii Dakta LUCY NKYA ametolea maelezo kuhusu dawa inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa KKKT, AMBILIKILE MWASAPILA kwamba bado Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya binadamu (NIMR) inaendelea na utafiti juu ya matibabu ya dawa hiyo.

Akijibu swali bungeni mjini Dodoma, Dakta NKYA amesisitiza kuwa dawa hiyo huponya kwa imani zaidi.

Aidha, Dakta NKYA amewataka waganga wote wanaotoa huduma za dawa asili kufika katika taasisi ya Kituo cha Tiba ya Asili ili kupata maelekezo ya ufanisi wa dawa wanazozitoa kudhibiti ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine.

Akijibu swali la Mheshimiwa KIDAWA SALIM kuhusu kujitokeza kwa waganga mbalimbali wanaodai kutibu ugonjwa wa kisukari, Dakta NKYA amesema waganga hao wa dawa za asili hawaruhusiwi kuitangaza dawa yoyote ambayo haijathibitishwa na NIMR.

/IS REPORTING 12




JUNI 30, 2011 ELIMU 7PM
DODOMA:

Serikali imeshauriwa kuunda Tume itakayochunguza vyanzo vya migomo na matatizo katika chuo kikuu cha serikali cha Dodoma (UDOM) ili kuhakikisha migomo inakoma chuoni hapo.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mjini Dodoma leo, Mbunge wa Jimbo la Rungwe Magharibi Profesa DAVID MWAKYUSA amesema serikali haina budi kutafuta suluhu ili wanafunzi waliofukuzwa chuoni hapo warejee darasani mapema.

Profesa MWAKYUSA pia amewataka wanasiasa kutowahusisha wanafunzi hao na mambo ya siasa badala yake wawaache wasome ili baadaye watumike katika kujenga nchi yao.

Amesema suala jingine la muhimu linaloweza kuwa suluhisho ya matatizo ya migomo chuoni ni kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wanafunzi kwa wakati na mlezi wa wanafunzi kuwa mwenye huruma na aliye karibu zaidi na wanafunzi hasa wakati wanapokuwa na matatizo.
Profesa MWAKYUSA amesema malumbano yanayoendelea hivi sasa juu ya migomo katika chuo hicho hayana tija yoyote iwapo suluhu ya matatizo hayo haitapatikana na kwamba pande zote zilizo katika malumbano hayo hakuna atakayeshinda.

/LC/IS REPORTING 15



JUNI 30, 2011 MKUTANO 7PM
MALABO:
Viongozi wa nchi za kiafrika wameanza mkutano wao wa kilele wa siku mbili leo katika mji mkuu wa Guinea ya Ikweta, Malabo, huku mgogoro wa Libya ukichukua nafasi kubwa katika mkutano huo.

Wawakilishi wa waasi nchini Libya pia wamealikwa kwenye mkutano huo.
Viongozi wa taifa waliopewa jukumu la mapigano yanayoendelea Libya, walikutana jana usiku, baada ya kutangaza mwishoni mwa juma lililopita kwamba Kanali MUAMMAR GADDAFI amekubali kutoshiriki katika mazungumzo ya kumaliza mzozo huo.

Viongozi hao wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanatarajiwa kuandaa mpango wa kumaliza mgogoro wa Libya baada ya kufunguliwa mkutano wa kilele mchana huu.

Waziri wa Libya anayehusika na masuala ya AFRIKA JONA IBRAHIM AMER amesema amewasili kuhudhuria mkutano wa kilele kutafuta uungaji mkono wa Umoja wa Afrika, katika wakati ambao utawala wake unaunga mkono mpango wa amani.

/IS NET/DW 14




JUNI 30, 2011 MGOMO 7PM
LONDON:

Kiasi cha waalimu Laki 6 nchini Uingereza wanatarajiwa kufanya mgomo katika mzozo kuhusu malipo ya uzeeni, na kusababisha kufungwa kwa shule na kuathiri usafiri katika mgomo mkubwa kabisa tangu serikali hiyo ya mseto kuchukua madaraka mwaka jana.

Mgomo huo wa siku moja dhidi ya mageuzi ya malipo ya uzeeni yanayotarajiwa kufanywa na serikali ya waziri mkuu DAVID CAMERON yanaweza kusababisha ucheleweshaji katika udhibiti katika vituo vya mpakani kwa watu wanaoingia Uingereza kupitia viwanja vya ndege, vituo vya treni na bandari.


/IS NET/DW 10









JUNI 30, 2011 ULEMAVU 7PM

DAR ES SALAAM:

Daktari Bingwa wa Uoni Hafifu kutoka nchini Marekani Dakta REBEKA KAMMER kupitia shirika lisilo la kiserikali la Under The Same Sun, amekabidhi vifaa mbalimbali vya macho kwa baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ili kuwawezesha kuona bila shida.

Akizungumza na waandishi wa habari jijni Dar es Salaam, Daktari huyo amesema sababu kubwa ya msaada huo ni kuwawezesha watanzania wenye matatizo ya kuona hasa walemavu wa ngozi, kukabiliana na tatizo hilo.

Dakta KAMMER amesema vifaa hivyo vitasaidia kutambua ukubwa wa miwani anayotakiwa kutumia mgonjwa wa macho ili kumsaidia asipatwe na matatizo zaidi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under The same Sun Bibi VICKY NTETEMA amesema kuwa vifaa vyote vilivyotolewa ni kwa ajili ya wanafunzi zaidi ya 300 wanaosomeshwa na mfuko wa hifadhi ya jamii nchini.




/EL/ES REPORTING

No comments: