Monday, August 29, 2011

HIVI, NINI LENGO LA KUJITANGAZA UNAPOTOA MSAADA?

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAMA PINDA ATOA ZAWADI YA IDD KWA WATOTO YATIMA DODOMA


MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ametoa zawadi ya Idd kwa vituo viwili vya Rahman Orphanage Centre na Kituo cha Huduma ya Neema na Uponyaji vinavyolea watoto yatima mkoani Dodoma.

Zawadi hizo zenye thamani ya sh. milioni 1.4, zilikabidhiwa jana mchana (Jumamosi, Agosti 27, 2011) kwa niaba yake na Mwangalizi wa Makazi ya Waziri Mkuu, Bw. Dickson Nnko.

Akipokea msaada huo, Katibu wa Rahman Centre, Bi. Rukia Hamisi alisema anamshukuru Mama Pinda kwa zawadi hizo kwani alikuwa hajui watoto hao wangekula nini wakati wa sikukuu.

Kituo hicho ambacho kipo eneo la Chang’ombe, kina watoto wapatao 80 ambao hufika na kushinda kituoni lakini ikifika jioni wanarudi kulala kwa ndugu zao.

Naye Mchungaji Musa Marwa, akipokea zawadi hizo kwa niaba ya Kanisa la Mennonite Tanzania, Dayosisi ya Kati, alisema anamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mama Pinda kwa zawadi hizo kwa sababu jambo walilolifanya ni kubwa kwa ajili ya watoto hao wenye uhitaji.

Kituo cha Huduma ya Neema na Uponyaji (Grace and Healing Ministry) ambacho kipo barabara ya kuelekea Iringa kilianza mwaka 2006 kikiwa na watoto 21 na sasa hivi kina watoto 100 wanaolelewa kituoni hapo.

Kila kituo kimepatiwa mbuzi mmoja, mchele (kg. 100), sukari (kg. 25), unga wa mahindi (kg. 25), unga wa ngano (kg. 25), mafuta ya kupikia (lita 20), katoni mbili za sabuni za miche, katoni mbili za sabuni za kuogea, mafuta ya kupakaa (dazeni mbili), biskuti (katoni mbili), pipi (pakiti sita), juisi (katoni tatu), majani ya chai na chumvi (katoni moja moja).

No comments: