Thursday, August 25, 2011

Ombi lingine kwa serikali.

Serikali imeombwa kuingilia kati mgogoro wa Chuo cha IMTU

Na Moshi Stewart

Maelezo

Dar es salaam

Uongozi wa Serikali ya wanafunzi wa chuo cha IMTU umeiomba serikali kuingilia kati migogoro mbalimbali inayowakabili wanafunzi chuoni hapo.

Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho Bw.Yared Chacha alisema wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipa ada kwa mfumo wa fedha za kigeni.



Bwana Yared Chacha alisema hivi karibuni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ilishapitia madai ya wanafunzi wa chuo hicho na kukiandikia barua chuo hicho kutumia mfumo wa malipo ya ada kwa fedha za Kitanzania.

Aliongeza kuwa licha ya chuo kupelekewa barua hiyo wanashangazwa mpaka sasa uongozi wa chuo hicho umekaidi maagizo ya TCU kitu ambacho kimeendelea kuwaumiza na kupelekea kufanya mgomo tarehe 18 Agosti 2011 kumshinikiza mwekezaji kuhusiana na suala zima la mfumo wa malipo ya ada kitu ambacho uongozi wa chuo uliendelea kukaidi.

Alisema kwa mwanafunzi wa taaluma ya udaktari amekuwa akilipa kiasi cha dola za Kimarekani 4500 kwa mwaka,taaluma ya uuguzi dola 3000 kwa mwaka na wanafunzi wa taaluma ya maabara wamekuwa wakilipa dola 2700- 3500 kwa mwaka.

Nae Rais mstaafu wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hico Bw.Jonas Mushi alisema zaidi ya wanafunzi 43 wa fani mbalimbali wapo nje ya chuo kwa sababu ya kushindwa kulipa ada kwa mfumo wa dola za kimarekani kitu ambacho kimesababisha usumbufu kwa wanafunzi hao.

“Zaidi ya wanafunzi 43 wameshindwa kulipa ada kwa mfumo wa dola za Kimarekani kitu ambacho kimesababisha usumbufu kwa wanafunzi hao”.Alisema Bw. Mushi.





No comments: