Sunday, September 11, 2011

SIMANZI KUBWA, BENDERA NUSU MLINGOTI, JK, DK SHEIN WAENDELEA KUPOKEA RAMBIRAMBI


KUMBUKUMBU za Watanzania jana zilirejea ajali ya meli ya mv Bukoba iliyozama katika
Ziwa Victoria Mei 21, 2006 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 400; kwa meli nyingine kuzama katika bahari ya Hindi na zaidi ya watu 163 kupoteza maisha.

Meli hiyo mv Spice Islanderwakiwamo watoto 60 waliokolewa. Ilikuwa ikisafiri kati ya Unguja na Pemba na kupata ajali hiyo eneo la Nungwi.


Habari za uhakika zinasema meli hiyo ilikuwa imebeba watu ambao walikuwa wanatoka mapumziko ya siku kuu ya Iddi.


Juhudi za kuopoa miili ya waliokufa zilikuwa zikiendelea jana huku Serikali ikiomba msaada kutoka nje ya nchi ili kusaidia uokoaji na uopoaji.


Ilielezwa jana kuwa Serikali ya Zanzibar ilianzisha kituo cha uokoaji na kutoa mwito kwa watu mbalimbali kushiriki katika uokoaji huku ikiomba msaada kutoka Afrika Kusini na Kenya.


Manusura wa ajali hiyo walikimbizwa bandarini kutoka eneo la tukio kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Khamis na kisha kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.


Miili ilikuwa ikisukumwa na mawimbi hadi ufukweni na hadi jana mchana maiti 100 walishaopolewa kwa mujibu wa mwandishi Ali Saleh wa BBC.


Maelfu ya ndugu na jamaa muda wote walikuwa wakisubiri taarifa za ndugu zao ambao huenda walikuwa ndani ya meli hiyo.


Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maafa, Mohammed Aboud, zaidi ya watu 100 hawakuwa wameonekana lakini manusura 325 waliokolewa huku 40 kati yao wakiwa

na hali mbaya za majeraha.

Mtalii wa Kiingereza, Catherine Purvis, aliyekuwa bandarini akisubiri boti ya kumpeleka Dar es Salaam, alisema alishuhudia miili mingi ikiopolewa majini.


“Niko hapa bandarini Zanzibar na watalii wenzangu 10 kutoka Uingereza na Marekani. Boti yetu imecheleweshwa, kwani zote zinatumika katika uokoaji.


“Watu wanapitishwa mbele yetu hapa wakiwa wamewekewa maji. Kuna pia miili mingi ya waliokufa,” alisema mtalii huyo alipokuwa akiwasiliana na BBC.


Rubani wa helikopta iliyotumika kutafuta miili, Neels van Eijik, alikwenda eneo la tukio. “Tulikuta manusura wameng’ang’ania magodoro, majokofu na chochote kilichoweza kuelea. Ni vigumu kuelezea idadi kamili, lakini naweza kusema kulikuwa na manusura zaidi ya 200 majini na baadhi ya maiti pia,” aliiambia BBC.


“Wakati huo, kulikuwa na boti chache zilizokwishaondoka. Zilikuwa zikitafuta manusura, lakini ingawa bahari haikuwa imechafuka sana bado mawimbi yalikuwa makubwa na hivyo

kuwa vigumu kuwaona.

“Tulisogelea boti na kuzielekeza waliko manusura ili wawachukue. Kulikuwa na maiti wachache majini.” Meli hiyo iliondoka Unguja kama saa 3 usiku na inasemekana ilizama kati ya saa 7 na 8 usiku.


Taarifa zilisema ilikuwa imebeba mizigo mingi huku baadhi ya abiria wakikataa kupanda kutokana na hali hiyo, manusura Abdallah Saied alikaririwa na Shirika la habari la Associated Press akisema.


Miongoni mwa waathirika wa ajali hiyo ni Khalifa Marhun, mkazi wa Manzese Tip Top jijini Dar es Salaam ambaye amepoteza ndugu wa karibu 11 kwa mpigo waliokuwa safarini kwenda

Pemba.

Marhun mwenye asili ya Konde, Pembe aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana kuwa, familia yake imeondokewa na ndugu wa karibu 11, wakiwemo wanane wa mke wake mkubwa

ambaye kwa sasa yuko Pemba.

“Ni maafa. Msiba mkubwa kwelikweli umetufika, ndugu 11 wamepotea katika ajali hiyo ya meli. Inauma sana…kuna ndugu wanane wa mke wangu mmoja,” alisema na kuongeza kuwa, kila mmoja alikuwa na safari yake, hivyo walikutana melini na kuzungumza mambo kadhaa, kabla ya kutokea kwa ajali hiyo ya kihistoria visiwani Zanzibar.


Dk. Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alieleza kuwa Serikali yake imejiandaa kuhudumia waliopatwa na maafa wakiwamo waliokufa na manusura.


Dk. Shein ambaye alifuatana na mkewe Mama Mwanamwema walifika Nungwi asubuhi ambapo pia, viongozi mbali mbali walihudhuria akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais, aalim

Seif Sharif Hamad, mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Balozi, viongozi wa vyama na Serikali na wananchi kutoka maeneo kadhaa.

Akizungumza na wananchi katika ufukwe wa Nungwi ambako baadhi ya maiti na majeruhi walikuwa wakiokolewa na kuopolewa, alieleza kuwa tukio hilo kubwa ni la kwanza kutokezea

Zanzibar na limeathiri familia na maendeleo ya nchi.

Alisema maeneo maalumu yameandaliwa kwa ajili ya kuhudumia majeruhi na marehemu.

Alieleza kuwa kwa waliookolewa hai wengine walipelekwa katika hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja kuchunguzwa afya na ambao afya zao si nzuri sana walipelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Dk. Shein aliwaomba wananchi kuwa watulivu na kuwapa nafasi madaktari ili watoe huduma kwa wananchi waliopata matatizo.


Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa taarifa rasmi kwa wananchi kila mara ili wajue hali inavyoendelea na kuwataka waandishi wa habari kushirikiana na Idara ya Habari, Maelezo,

kwa ajili ya taarifa sahihi.

Dk. Shein alisema jitihada za Serikali zinaendelea kuchukuliwa kwa ushirikiano na vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vikiwamo vya SMZ na vya Jamhuri ya Muungano.


Aidha, alisema madaktari kutoka taasisi na mashirika ya maafa yakiwamo ya Msalaba Mwekundu wanaendelea kutoa ushirikiano katika kuhudumia majeruhi.


Dk. Shein alisema kikao maalumu cha Serikali kilitarajiwa kufanyika jana Ikulu mjini Zanzibar kuzungumzia tukio hilo.


Akiwa Nungwi Dk. Shein aliwaangalia na kuwapa pole wale manusura wakiwamo watoto, vijana na wazee. Pia, alifika Kivunge kuwapa pole majeruhi.


Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka eneo hilo, Dk. Shein alisema Serikali amejipanga vizuri na ndiyo maana ikaunda Kamati Maalumu ya Maafa ili kukabiliana na hali hiyo.


Aidha, alisema kutokana na Zanzibar kuwa sehemu ya Muungano, ndio maana imeona haja ya kupata nguvu za ziada kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi ili kusaidia juhudi za uokoaji na uopoaji.


Mapema akitoa taarifa kwa Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Juma Khamis, alisema mapema asubuhi waliokolewa baadhi ya watu na kupelekwa Kivunge.


Mkuu wa Mkoa pia, alieleza kuwa vyombo vya majini vilifika eneo la tukio na kusaidia kuokoa ikiwamo boti ya Sea Express ambayo iliokoa watu 259 na kuopoa maiti 49 na baada ya hapo ilielekea bandari ya Malindi baada ya kushindwa kufunga gati Nungwi.


Hadi Rais anaondoka Nungwi juhudi za uokoaji zilikuwa zinaendelea na majeruhi walikuwa wakipelekwa eneo lililotengwa kwa ajili ya huduma za afya.


Salamu za JK

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Shein kwa msiba huo.

Katika salamu hizo, Rais Kikwete alisema: “Nimepokea kwa mshtuko, masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya ajali na kuzama kwa meli ya mv Spice Islander.


“Kutokana na kuzama huko, abiria wengi wamepoteza maisha na walionusurika wamepata athari zifanyazo afya zao kuhitaji uangalizi wa karibu.


Aidha mali nyingi zimepotea. “Haya ni maafa makubwa kwa nchi yetu na Watanzania wote wako pamoja na ndugu zao wa Unguja na Pemba katika kipindi hiki kigumu.


Kwa niaba yao nakutumia salamu za mkono wa pole na kupitia kwako naomba unifikishie salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopoteza ndugu na jamaa zao.”


Rais aliomba wafahamu kuwa msiba wao ni msiba wa Watanzania wote, majonzi yao ni ya wote na uchungu wao ni wa wote.


Aliwaombea moyo wa subira na uvumilivu na kuungana nao kuwaombea marehemu kwa Mola awape mapumziko mema, awasamehe madhambi yao na kuwajaalia pepo.


“Kwa ndugu zetu walionusurika katika ajali hiyo, tunawapa pole kwa msukosuko mkubwa walioupata. Tunaungana nao kumshukuru Mwenyezi Mungu kuokoa maisha yao na tunawaombea wapone upesi ili waweze kuendelea na juhudi za kujiletea maendeleo yao na

kuijenga nchi yetu.”

Rais alisema: “Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nakuhakikishia ushirikiano wangu binafsi na wa wenzetu wote katika hatua zote za kukabiliana na janga hili na athari zake. Tutakupa kila aina ya msaada utakaohitaji tutoe.”


Inspekta Jenerali

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Saidi Mwema, aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati huu ambapo uokoaji wa watu waliopata ajali ukiendelea.

Alisema hadi jana saa 7.30 mchana watu 525 walikuwa wameokolewa wakiwa hai na 62 wakiwa wamefariki dunia.


Mwema alisema kazi ya upelelezi na kujua chanzo cha ajali hiyo bado inaendelea kwa kuhusisha Polisi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mamlaka ya Bandari, Kikosi cha KMKM na vinginevyo.


Alisema mbali na vikosi hivyo pia viliundwa vikosi vingine vinne tofauti vitakavyokuwa

vikishughulika na utoaji wa taarifa, utambuzi na uratibu wa maafa hayo.

Aidha, alisema taarifa kamili kuhusu chanzo cha ajali hiyo itatolewa baada ya upelelezi kukamilika.


Mv Bukoba

Usiku wa Mei 21, 1996, watu wapatao 400 walipoteza maisha katika ajali ya kuzama kwa meli ya mv Bukoba katika Ziwa Victoria. Meli hiyo ilizama wakati ikikaribia kutia nanga katika bandari ya Mwanza ikiwa safarini kutoka Bukoba.

Meli hiyo siku hiyo ilibeba abiria wapatao 700 na mizigo ya tani 850. Hiyo ilikuwa ni ajali kubwa kuwahi kutokea katika historia ya ajali za majini nchini.


Katika ajali hiyo, ilikuwa vigumu kujua idadi kamili ya waliokufa wakiwamo wageni kwa sababu orodha ya abiria katika daraja la kwanza na la pili walikuwa watu 443 wakati katika daraja la tatu ambalo nauli yake ilikuwa chini na hivyo kubeba watu wengi halikuwa na

orodha.

Hata hivyo ripoti ilibaini kwamba Waganda 10 walipoteza maisha huku familia moja ya Tanzania ikipoteza ndugu 25 na kwaya ya shule ikipoteza watu 15.


Hata hivyo, baada ya kazi ya uopoaji kuwa ngumu, Serikali ilitangaza rasmi maziko kufanyika ndani ya meli hiyo na taarifa za mwisho kusema inakadiriwa watu waliopoteza maisha kuwa takriban 1,000.


Maofisa tisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) walishitakiwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, kwa kusababisha vifo hivyo vya mamia ya watu katika ajali hiyo.


Nahodha wa meli hiyo, JumanneRume Mweru, alisimamishwa kazi na Serikali pamoja na Meneja wa TRC divisheni ya safari za majini, Cleophas Magoge na wengine sita ili kupisha uchunguzi.


Sababu za kuzama kwa mv Bukoba ilikuwa ni kujaza abiria na mizigo kuzidi uwezo wake.


Wakati huohuo, kutokana na msiba mkubwa uliotokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander katika bahari ya Hindi usiku wa kuamkia jana, Rais Kikwete ameahirisha ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Canada ambako alikuwa amealikwa na Gavana Mkuu wa nchi hiyo, David Johnston.


Katika ziara hiyo iliyokuwa ifanyike kuanzia Jumatano ijayo, Rais angekutana pia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Stephen Harper. Rais ameiomba Serikali ya Canada kupanga ziara hiyo kwa tarehe za baadaye.


Wakati tunakwenda mitimboni, habari kutoka Zanzibar zilidai idadi ya waliofariki ilikuwa imefikia 200, wakati waliookolewa wakifikia 606.
CHANZO: HABARI LEO 

No comments: