Wednesday, October 12, 2011

WARIOBA AWATAKA WATZ WACHAPE KAZI

JAJI WARIOBA AWAONYA WATANZANIA WAACHE KULALAMIKA
*Asifu juhudi za Serikali kuleta maendeleo
 
WAZIRI MKUU Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba amesifu jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo nchini lakini amewaonya Watanzania waache tabia ya kulalamikia kila jambo na badala yake wafanye kazi.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Oktoba 11, 2011) wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
 
Amesema kuna mambo mengi ambayo yamefanyika tangu nchi ipate uhuru lakini hakuna anayetambua mchango huo na badala yale kila mmoja amekuwa mwepesi wa kutoa lawama. “Kuna kitu kimoja kinachonipa matatizo nacho ni kuona nchi imekuwa ni ya watu waliokata tamaa… wananchi na viongozi ni watu wa kulalamika tu, sisi sote ni walalamikaji,” alisema mbele ya waandishi hao.
 
“Kwa hali ilivyo, nasema tujihadhari kwa sababu tunaweza kupata matatizo ya kiuchumi kwa sababu ya matatizo ya umeme, bei kubwa ya mafuta na kushuka kwa thamani ya shilingi. Kama shilingi itaendelea kushuka, mfumuko wa bei utakuwa mkubwa na atakayeumia ni mwananchi wa kawaida,” alibainisha.
 
Alisema kazi ya kutafuta uhuru ilikuwa ngumu na kulikuwa na baadhi ya watu walioamini kuwa Tanganyika isingepata uhuru wake kwa sababu kazi ya kumtoa Mwingereza haikuwa rahisi. “Mimi ni mmoja wa watu waliokuwepo uwanjani kushuhudia bendera ya Mwingereza ikishusha na kuona bendera ya Tanganyika ikipandishwa.”
 
“Jeuri tuliyokuwa nayo wakati wa harakati za kutafuta uhuru ilikuwa kubwa… dhamira tuliyokuwa nayo ibaki vilevile, tuwe ni watu wa kuthubutu. Kama tuliweza wakati ule, tukiwa hatuna hatuna teknolojia za kisasa kama sasa, naamini hakuna kitu kinachoweza kuturudisha nyuma,” alisisitiza.
 
Alisema umefika wakati wa wananchi kukaa pamoja na kujadili changamoto zinazolikabili Taifa na kukubali kuwa matatizo siku zote yapo. “Matatizo ni sehemu ya maisha, ukithubutu kuyapatia ufumbuzi unaweza kupata suluhu ya matatizo hayo. Maonesho haya yanatukumbusha jinsi tulivyoweza kuthubutu, yanatukumbusha tulikotoka,” alisisitiza.
 
(mwisho)
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021
DAR ES SALAAM

No comments: