Saturday, February 12, 2011

KILICHOTOKEA MISRI, KINA FUNZO LOLOTE KIIMANI, KISIASA AU KIMAPINDUZI?




Wengine wanadai ni funzo kwa watawala dhalimu wa Afrika ambao wamezoea kuendesha nchi zao kama nyumba zao ndogo.

wengine wametaja Aljeria, Libya, Zimbabwe na kwingineko, lakini tuangalie kwa makini, kilichotokea Misri kina funzo gani kwa dunia na Afrika kwa ujumla?

Baada ya wamisri kuchoshwa na utawala wa kifalme ambao uliwanyanyasa kwa maelfu ya miaka, tukianza na mfalme Farao, hatimaye katika miaka ya 1950, Wamisri walikataa utawala wa kifalme.

Baada ya nguvu ya umma kutumika kumaliza utawala wa kifalme ni wanajeshi ndiyo waliendelea kupinduana na kunyang'anyana madaraka ya nchi hiyo.

baadaye Misri katika miaka ya 1980 ilijikuta katika mikono ya Mohamed Hosn Mubarak, mwanajeshi aliyekuwa amefuzu katika urushaji wa ndege za kivita, lakini aliyekuwa amepanda cheo hadi kufikia mkuu wa kitengo cha ndege cha jeshi la nchi hiyo, na hatimaye mkuu wa majeshi.

Baada ya miaka 30, Mubarak ni kama akawa amelewa madaraka ya muda mrefu aliyoyahodhi. Ikaripotiwa kuwa anamwandaa mwanaye Gamal kuwa Rais wa nchi hiyo baada ya baba kuachia ngazi.

Wakati hayo yakitokea, hali ya mambo ndani ya misri ikawa tete, UKOSEFU wa AJIRA ukawa unazidi kila siku, BEI ya CHAKULA ikapaa kiasi cha kuonekana kama chakula ni starehe, bei ya MAFUTA na UBOVU wa HUDUMA za JAMII ukahanikiza shida za wamisri.

Wengi wakajiuliza, jibu walilopata ni kubadilisha utawala, licha ya tambo nyingi na ubabe wa Rais HOSN MUBARAK, hatimaye wananchi wamefanikiwa kumng'oa.

Wengi wanahusianisha kilichotokea Misri na mustakabali wa amani ya Mashariki ya Kati, ikikumbukwa kuwa Mubarak alikuwa mhimili mkubwa wa Israel katika kuhakikisha kuwa Israel haihujumiwi, hasa na wanamgambo wa kiislamu wa kundi la Hamas linalotawala katika Ukanda wa Gaza.

Uwanja huu ni huru kwa ajili ya kuchangia chochote unachokijua kumhusu Mubarak, Siasa za Misri, husianisha na Israel, na amani ya Mashariki ya Kati, uhusiano na Marekani, Saudi Arabia na mataifa mengine ya kiarabu.

No comments: