Thursday, February 10, 2011

PINDA NA MASWALI YA PAPO KWA PAPO. JE NI KUTETEA CHAMA? AU KUJIPAKA MATOPE ZAIDI?




Waziri Mkuu MIZENGO PINDA amesema vifo vya raia watatu vilivyotokea Arusha mjini hivi karibuni, baada ya Polisi kufyatua risasi kutawanya maandamano ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vingeweza kuepukika.

Hali kadhalika, Mheshimiwa PINDA amesema serikali inamtambua Meya wa Arusha, aliyechaguliwa kihalali na wajumbe wa baraza la madiwani wa halmashauri ya Arusha, licha ya Naibu Meya kutoka Chama cha TLP, kutangaza kujiuzulu wadhifa huo kupitia vyombo vya habari.

Amesema kama Mwenyekiti wa CHADEMA, FREEMAN MBOWE na chama chake wangeamua kushirikiana na vyombo vya usalama kama walivyokubaliana, mauaji ya Arusha yasingetokea.

Mheshimiwa PINDA ameelekeza lawama kwa CHADEMA kwa kile ambacho amekiita kushindwa kutimiza makubaliano yake na jeshi la polisi na kuandamana kwa lazima hivyo kusababisha vifo hivyo kutokea na kwamba kwa kufanya hivyo, chama hicho kimeshindwa kujenga chama kwa misingi ya amani na hivyo kupoteza sifa ya kuaminiwa na wananchi.

Mheshimiwa PINDA amesema hayo wakati akijibu maswali ya papo kwa papo leo bungeni mjini Dodoma.

pichani-mmoja wa marehemu wa sakata la Arusha.

Akilielezea Bunge kuhusu kilichotokea katika uchaguzi wa Meya wa Arusha na Naibu Meya, Waziri Mkuu PINDA amesema uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu hivyo serikali inawatambua viongozi hao kama viongozi halali na kwamba yeyote mwenye pingamizi nao yuko huru kwenda mahakamani.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu PINDA ametoa wito kwa watanzania kutumia chakula kwa uangalifu kutokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kubainisha kuwa kwa wastani, nchi itakabiliwa na upungufu wa mvua katika msimu ujao.

Ameeleza kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa inasambaza mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi ili kuwaepushia wananchi gharama za kupanda kwa maisha kutokana na hali hiyo.

Baada ya kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kumalizika, Mbunge wa Arusha mjini kupitia Chadema, GODBLESS LEMA alisimama na kutaka mwongozo wa spika kwa mujibu wa kanuni ya 68 ya bunge, kipengele cha 7, akitaka mwongozo wa kile mbunge anachotakiwa kufanya endapo kiongozi mwenye wajibu mkubwa serikalini kama Waziri Mkuu anaposema uwongo bungeni.

Hata hivyo, Spika ANNE MAKINDA amemtaka mbunge huyo kuthibitisha kauli yake katika kipindi cha siku 14, vinginevyo ataadhibiwa na spika kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

No comments: