Monday, February 7, 2011

Vichanga zaidi vyatelekezwa Mwananyamala!!


Baadhi ya wagonjwa wakiwa katika wodi ya akinamama, hospitalini Mwananyamala.


SIKU moja baada ya kamati iliyoundwa na serikali kuanza kuchunguza tukio la miili 10 ya vichanga kufukiwa shimo la taka, ndani ya makazi binafsi, jirani na Hospitali ya Mwananyamala, miili mingine ya watoto wachanga imetelekezwa na wazazi kwenye hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizofikia Blog ya Mwerevu na kuthibitishwa na uongozi wa hospitali hiyo, mwanamke mmoja ambaye taarifa zake zilipelekwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, alijifungua mtoto kabla ya wakati, mimba ikiwa na umri wa miezi sita na kutoroka wodini kabla ya kukabidhiwa maiti ya mtoto wake.

Mwanamke mwingine aliyepatwa na tatizo kama hilo la uzazi, alielezwa kuwa alizuiwa kutoroka hospitalini hapo, baada ya kueleza nia yake ya kutaka kulipa fedha ili maiti ya mtoto wake ibaki hospitalini hapo kwa maziko.

Taarifa hizo ambazo zimedhibitishwa na hospitali hiyo, zinaeleza tangu kubainika kwa miili ya vichanga hivyo ndani ya shimo la taka, Jumatatu wiki hii na hospitali hiyo kuingia kwenye msukosuko, kuna miili zaidi ya kumi imehifadhiwa chumba cha maiti, huku wazazi wakiwa wametoweka.

“Matukio hayo mawili ni ya leo hii, tukizungumzia hali ilivyo tangu Jumatatu mpaka leo (Alhamisi), kuna miili ya watoto wachanga ambayo imekimbiwa na wazazi inatunzwa mochwari,” kiongozi mmoja Hospitali ya Mwananyamala.

Inadaiwa mtumishi wa kuhudumia chumba cha kuhifadhia maiti, anaendelea kushikiliwa polisi kwa mahojiano.

Wakati huohuo, Balozi wa Uzazi Salama Tanzania, Stara Thomas, amesema atafuatilia kwa makini kamati ya kuchunguza tukio hilo ili kujua kiini cha vifo ya watoto husika.

Thomas alisema inawezekana uongozi wa hospitali unafahamu mambo mengi zaidi kwa kuwa, jamii imegundua hili baada ya watoto hao kukutwa kwenye shimo.

Alisema wajawazito wanapokuwa na shaka kuhusu jambo lolote wanatakiwa kuuliza kwa kuwa, ni haki yao ya msingi na wakiona hawatendewi haki wapaze sauti zao sehemu husika.

Alitaka serikali kuangalia mafunzo ya wahudumu wa afya na kutimiza mishahara yao kikamilifu, kuepuka matatizo ya aina hiyo na kwamba, linapobainika tatizo linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi haraka.

Kwa mujibu wa Thomas, zipo hospitali nyingi ambazo zinalalamikiwa kutoa huduma kwa wajawazito, ikiwamo Mwananyamala na nyingine ambazo bado anazifanyia uchunguzi.

Katika tukio lingine, Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC), imesema wiki ijayo itatoa majibu sahihi ilipo miili ya watoto wanne mapacha wa Shija Maige.

Akizungumza kwa simu jana, Muuguzi mkuu wa hospitali hiyo, Viola Munishi, alisema tayari wamefanya jitihadi za kutoa maelezo ilipo miili ya watoto hao na ofisi yake imeshirikiana na ofisi ya ustawi wa jimii ya Bugando.
Munishi alisema maelezo yote yatapatikana ofisi za ustawi wa jamii Bugando.

Maige ambaye ni mama wa watoto hao na mumewe walidai kuwa, hawajui ilipo miili ya watoto wao na kwamba, waliambiwa watoe Sh3,000 ili waonyeshwe au Sh500,000 kusafirishiwa maiti hizo.

mwananchi.

No comments: