Friday, September 9, 2011

BUNGE LATOA UFAFANUZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA

Simu Na. 022 2112065/7
Fax Na. (255) 022 2112538
E-mail:  tanzparl@parliament.go.tz  mailto:ParlDom@bunge.go.tz


  
S.L.P. 9133
DAR ES SALAAM
 TAARIFA KWA UMMA
YA: UFAFANUZI KUHUSU HABARI YA GAZETI LA TANZANIA DAIMA LA
TAREHE 5/9/2011 ILIYOSEMA “UCHUNGUZI UDA KUANZA LEO”
Katika  Gazeti  la  Tanzania  Daima  la  tarehe  5  Septemba  2011  lilichapisha
habari yenye kichwa kilichosomeka “Uchunguzi UDA kuanza leo”  ikieleza
kuwa kamati iliyoundwa na Bunge kuchunguza kashfa ya uuzwaji wa Shirika
la Usafiri Dar es salaam (UDA) ilitarajia kuanza kazi yake siku ya Jumatatu 5
Septemba 2011  chini ya uwenyekiti wa Mhe. Murtaza Mangungu, Mbunge wa
Kilwa Kaskazini CCM.
Ofisi ya Bunge inapenda kutoa taarifa kwa vyombo vya Habari na Umma kwa
ujumla  kuwa  taarifa  hiyo  ni  potofu  na  haina  ukweli  wowote.  Ukweli  ni
kwamba mpaka sasa hakuna kamati yoyote ya Bunge inayochunguza suala la
uuzwaji  wa  Shirika  la  Usafiri  Dar  es  salaam  (UDA).  Ikumbukwe  kwamba
wakati wa Bunge la Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya
Umma Mhe. Zitto Kabwe (Mb) aliongea na waandishi wa Habari kuhusu nia ya
Kamati  yake  kufanya  uchunguzi  huo  ikiwa  ni  pamoja  na  mapendekezo  ya
wajumbe aliyowasilisha kwa Mhe. Spika kwa lengo la kupata kibali chake kwa
muibu wa Kanuni za Bunge.
Aidha,  ifahamike  kuwa  uamuzi  wa  Mhe.Spika  kuhusu  suala  hilo  ulikuwa  ni
kuliacha  lichunguzwe  na  Mdibiti  na  Mkaguzi  Mkuu  wa  Hesabu  za  serikali
(CAG)  na  baadae  CAG  awasilishe  taarifa  ya  uchunguzi  wake  Serikalini  na
hatimaye Bunge liarifiwe matokeo ya Uchunguzi huo kupitia Serikali
Hata  hivyo  ieleweke  kuwa,  Kwa  mujibu  wa  Kanuni  za  Kudumu  za  Bunge,
Toleo la 2007, Kanuni  ya 117, inaeleza kuwa Bunge linaweza kuunda Kamati
Teule  kwa  madhumuni  maalumu  kwa  hoja  Mahususi  itakayotolewa  na
Kuafikiwa Bungeni. Na fasili ya (4) inasema kuwa wajumbe wa kamati Teule
watateuliwa  na  Spika  na  watamchagua  Mwenyekiti  wa  Kamati  hiyo  kutoka
miongoni  mwao.  Pili,  kanuni  ya  114  (3)  inatamka  bayana  kuwa  kamati  ya
kudumu  itakutana  kila  inapoitwa  na  Spika,  Naibu  Spika  au  na  Mwenyekiti
wake baada ya kupata idhini ya Spika
Mwandishi wa habari hiyo, hakufuatilia uhalali wa kile alichokusudia kuandika
na hata kujiridhisha na utaratibu wa kamati zinavyofanya kazi kwa mujibu wa
kanuni na badala  yake aliandika maoni yake kwa jinsi alivyohisi. Hili ni jambo
la hatari!
Mwisho,  tunapenda  kuwakumbusha  waandishi  wote  wa  Habari  kuzingatia
miiko  ya  kazi  yao  na  kuwa  makini  waandikapo  jambo  lolote  kwa  wasomaji
wao,   kwani   wasipofanya   hivyo   na   kuandika   habari   za   kupotosha,
wanasababisha   usumbufu   usio   wa   lazima   na   wanaweza   kulaumiwa
kusababisha mikanganyiko miongoni mwa jamii yetu.
Ofisi  ya  Bunge  inapenda  kuwaarifu  wananchi  wote  wakiwemo  wanahabari
kuwa Idara yake ya Habari imekuwa ikitoa na itaendelea kutoa ushirikiano wa
kutosha kuwaarifu waandishi kuhusu taarifa zozote wanazohitaji na hususani
wanazotaka kuandikia habari. Aidha, tunasikitishwa na uandishi wa namna hii
wa  kuandika  kwa  kutegemea  hisia  bila  hata  kufanya  jitihada  za  kutosha  za
kuwasiliana na Ofisi ya Bunge.
Ofisi   ya   Bunge   iko   wazi   kutoa   ushirikiano   kwa   ufafanuzi   wowote
utakaohitajika.

Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ndogo ya Bunge
Dar Es Salaam
8 Septemba 2011  


No comments: