Friday, September 9, 2011

VIJANA MMEMSIKIA FIRST LADY??

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka vijana hapa nchini kufanya kazi kwa bidii kwani wao ni chachu ya maendeleo na kuepukana na dhana kuwa ukikaa bila ya kufanya kazi utapata mafanikio katika maisha.
 
Mama Kikwete  aliyasema hayo jana wakati akiongea na Ushirika wa Vijana wa Kikristo wa Uzalishaji Tanzania (UVIKIUTA)  mara baada ya kumaliza kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na vijana hao huko Mbagala jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa maisha bora yanawezekana kwa kila mtanzania kwa kuhakikisha kuwa vijana wana ari na moyo wa kufanya kazi ili kuleta maendeleo katika nchi kwani vijana wananguvu za kutosha ukilinganisha na wazee ndiyo maana Serikali na mashirika binafsi  wanahakikisha kuwa vijana wanapata elimu, afya bora na kuwaunga mkono pale ambapo hawawezi kupafikia kwani ni rahisi kusaidia kundi kuliko mtu mmoja mmoja .
“Hivi sasa vijana wengi wanafikiria kuwa ukikaa bila ya kufanya kazi utafanikiwa kimaisha mimi nawaambia kuwa hakuna kitu kama hicho, ninachowasihi mfanye kazi kwa ushirikiano na kujituma hakika mtafanikiwa kwani hata vitabu vya dini vinasema kuwa utakula kwa jasho lako”, alisema Mama Kikwete.
Mke huyo wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliendelea kusema kuwa anawajibu mkubwa  kwa jamii ndiyo maana anafanya kazi ya kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana hasa wanawake na vijana.
Mama Kikwete alisema, “Mnapokea vijana wengi kutoka nchi mbalimbali ambao wanakuja kujifunza kutoka kwenu nanyi mnaenda kujifunza kwao (exchange programme) kwa kuwa kuna  vitu vizuri  vinafanywa kwa vijana wa Tanzania ndiyo maana wanakuja nawasihi muendelee na moyo wa ushirikiano ili muweze kujifunza na kufahamu mambo mengi zaidi .
Kwa upande wa utunzaji wa mazingira Mama Kikwete alisema kuwa kazi inayofanywa na Ushirika huo ni nzuri kwani hivi sasa kuna uharibifu mkubwa wa mazingira lakini kama jamii nzima itaamua kujitolea na kuyatunza nchi itaepukana na janga la ukame.
Akisoma taarifa ya UVIKIUTA Mwenyekiti wa Ushirika huo Benedict Mongi alisema kuwa malengo ya kuanzishwa kwa Asasi hiyo ni kuendeleza Elimu na ujuzi kwa vijana wa kike na wa kiume, kuwezesha uanzishaji wa ajira na kuwezesha ushirika wa vijana na jamii katika kazi za utunzaji wa mazingira.
Mongi aliyataja mafanikio waliyoyapata hadi sasa kuwa ni mradi wa kijiji cha mazingira ambao umewawezesha kujenga makazi ya kudumu ya nyumba tisa kwa wanachama wake, kuweka miundombinu ya barabara zenye mzunguko wa kilomita saba kwa kiwango cha kokoto, kujengwa kwa kisima cha maji, kuanza kwa ujenzi wa kutuo cha Afya na kupanda miti 10000 katika hifadhi za barabara ya kijiji na vianzo vya maji.
“Elimu ya maendeleo imetoa fursa kwa vijana kutoka nchini na nje ya nchi kukutana na kubadilishana ujuzi, stadi na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo hadi sasa zaidi ya vijana 4740 kutoka nchi za Kenya, Afrika ya Kusini, Msumbiji, Finland, Ujerumani, Uholanzi, Italy, Korea ya Kusini, Ireland, Canada, Asia na Marekani  wamepata fursa ya kushiriki katika makambi ya vijana ambayo yameleta mafanikio  makubwa katika maisha yao”, alisema Mongi.
UVIKIUTA ni taasisi ya Maendeleo ya vijana ambayo ilianzishwa mwaka 1983 kufuatia wito wa Taifa uliomtaka kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi kufanya kazi. Serikali ya wakati huo kupitia program yake ya nguvu kazi ilitaka kuwaona vijana wakijiunga kwa pamoja na kuanzisha shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwaondoa katika umaskini , ujinga na maradhi.

No comments: