Friday, February 4, 2011

Tanzania

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka historia ya kuwa nchi ya kwanza duniani kuandaa Mpango wa Pamoja wa Maendeleo kwa kushirikiana na Mashirika Manne yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UM).

Mashirika hayo ni Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP),Shirika la kuhudumia watoto (UNICEF), Mpango wa Chakula Duniani(WFP) na Shirika linalohusika na Idadi ya watu (UNFPA).

Kufuatia kukamilishwa kwa mchakato huo wa aina yake, Jumuia ya Kimataifa imeipongeza na kuisifu Serikali ya Tanzania kwa kuonyesha njia na kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine.



Mpango huo ambao unajulikana kama Common Country Programme Document (CCPD),umewasilishwa mbele ya Bodi tendaji za UNDP na UNFPA na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Dakta SERVACIUS LIKWELILE ukiwa ni sehemu ya Mpango Mkubwa wa Umoja wa Mataifa.



Bodi Tendaji za Mashirika hayo zimekuwa zikiendesha mikutano yao ya kikazi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York ambapo tanzania ilipatiwa fursa ya kuwasilisha Mpango huo.

Utekelezaji wa CCPD utafanyika kwa miaka minne kuanzia Julai 2011 hadi June 2015,ambapo Tanzania kupitia mpango huo itapata Dola za Kimarekani 773 milioni zitakazotolewa na Umoja wa Mataifa.

No comments: